Share news tips with us here at Hivisasa

Vijana walio kwenye vyuo vikuu na taasisi za masomo kutoka eneo la wadi ya Bomariba, eneo bunge la Bonchari wanamtaka mbunge wao Zebedeo Opore kuongeza kima cha hela wanachopokezwa kutoka akiba ya basari ya karo vyuoni.

Kwenye mahojiano na mwandishi huyu siku ya Jumanne chuoni Kisii, kiongozi wa chama cha wanafunzi kutoka eneo bunge hilo Isaac Motari alidai kuwa kiwango wanachopata ni kidogo mno, na mara nyingi hakiwatoshelezi kwenye mahitaji ya ulipaji karo.

Kiongozi huyo aliongeza kusema kuwa baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakipewa kati ya shilingi 3,000 na elfu 5,000, na kumtaka mbunge wao kuangalia swala hilo na kuongeza kiwango hicho hadi shilingi elfu kumi na tano ili angalau kukidhi mahitaji.

"Pesa tunapewa kama karo ni kidogo mno, elfu tatu au tano haitoshi kitu, namsihi mbunge wetu kuongeza kiwango hicho hadi elfu 15,000 ili ziweze kuwakimu vizuri sababu hizi zinatolewa hazitoshi," alisema Motari.

Vile vile, aliwasihi viongozi wa siasa kutoka eneo hilo kuwasaidia vijana ambao wanataka kuendelea na masomo kwa kuwafadhili kielimu na kufanya maendeleo ili kupunguza hali ya umasikini kwenye sehemu hiyo.

Alisema kuwa atajitahidi kuona kuwa kila kijana ambaye ako chuo anapata haki ya pesa ya karo kutoka akiba ya pesa ya maendeleo ya eneo bunge, CDF.