Wanafunzi wa shule za upili wamehimizwa kuepukana na utumizi wa mihadarati kama njia ya kujenga maisha bora na jamii thabiti ya siku za usoni.
Akihutubia wanafunzi kwenye kongamano la vyama vya wanafunzi wa kiislamu vya shule za upili katika shule ya upili ya Mtwapa Elite siku ya Jumamosi, mwenyekiti wa chama cha wanafunzi wa kiislamu wa shule hiyo Abubakar Asbathu aliwasihi wenzake kujiweka mbali na jinamizi hilo linaloendeleya kuangamiza vijana nchini.
Aidha, amewataka wanafunzi wenzake wajifunze elimu ya dini kwani ndio msingi wa kuongoka ulimwenguni na kujikurubisha kwa mola wao.
Kwa upande wake, Ustadh Said Salim aliwataka wanafunzi hao kuwa na tabia nzuri kwani ndio ufunguo wa kila jambo jema.
Vile vile, aliongeza kuwa vijana ndio uti wa mgongo wa jamii, watakapoimarika, itaimarika jamii na kinyume chake ni kulemaa nyuma jamii nzima.
Watahiniwa wa kidato cha nne wanaanza mtihani wao siku ya Jumatatu kama walivyopanga maafisa wa baraza la mitihani nchini.
Awali kulikuwa na ati ati ya mtihani hao kusongezwa mbele kwa sababu ya mgomo wa walimu uliodumu kwa wiki tano.