Wanafunzi katika chuo kikuu cha Maseno sasa wanaishi kwa hofu kwa sababu ya mzozo kuhusu mipaka unaoendelea kutokota kati ya viongozi wa kaunti mbili.
Wanafunzi wengi wanahofu kuwa iwapo mzozo huo utaendelea, basi hali ya usalama itadorora zaidi ikilinganishwa na hapo awali ambapo kumekuwa na mavamizi ya wanafunzi kila siku.
Wanafunzi walioongea na wanahabari wametaka viongozi wa Kaunti za Kisumu na Vihiga kuchukua hatua na kusuluhisha tatizo hilo haraka iwezekanavyo ili amani iliyoshuhudiwa hapo awali irejee kikamilifu.
"Ikiwa mzozo huu hautatatuliwa, tutaendelea kuvamiwa zaidi," alisema Joseph Mundia, mwanafunzii wa mwaka wa nne chuoni humo akiongeza kuwa viongozi kutoka pande zote mbili wanafaa kuchukua hatua za mapema kabla ya mambo kuharibika.
Eneo la Maseno limekuwa liking'ang'aniwa na viongozi kutoka kaunti ya Kisumu na wenzao wa kaunti ya Vihiga kuhusu ni wapi eneo hilo lipo kati ya kaunti hizo mbili.
"Serikali iingilie kati haraka iwezekanavyo kutatua mzozo huo. Hatutaki kuishi kwa wasiwasi," alidakia Leila Mitei, mwanafunzi wa mwaka wa tatu anayesomea uanahabari.
Haya yanajiri huku wanafunzi wengi wakilazimika kuishi nje ya shule kwa ukosefu wa nyumba za kutosha chuoni mwao na sasa wanafunzi hao wamekitaka kitengo cha usalama kuchukua hatua ya kufanya ziara za usiku ili kupunguza visa vya mavamizi ambayo yamekuwa yakitokea.