Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wanaharakati wa kutetea mswala ya ardhi nchini wamelishinikiza bunge la kitaifa kupitisha mswada wa kuivunjilia mbali tume ya kitaifa ya ardhi nchini kwa kushidwa kutatua mizozo ya ardhi.

Kulingana na Mwenyekiti wa kitaifa wa Shirika la ardhi la ‘Residents Land protection Organisation of Kenya’ Dewelly Nyambu, tangu tume hiyo kubuniwa haijatatua kesi hata moja ya mizozo ya ardhi licha ya shirika hilo kuwasilisha kesi za ardhi mbele ya makamishna wa tume hiyo.

Katika mahojiano na mwanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Nyambu alisema kwamba kuvunjwa kwa tume hiyo huenda kukasadia pakubwa kurekebisha mizozo ya ardhi kwani makamishna walioteuliwa kusimiamia tume hiyo wameshindwa kuwajibikia majukumu yao kikamilifu na kusababisha kufurushwa kwa wakazi katika ardhi zao.

“Tunaunga mkono kikamilifu kuvunjwa kwa tume ya kitaifa ya ardhi kwa kushindwa kuwajibikia majukumu yake jinsi ipaswavyo. Imesababisha matatizo mengi tangu tume hii ibuniwe kwa sababu hapo awali mahakama ilikuwa ikitatua mizozo ya ardhi mashinani, lakini sasa imewachiwa tume sio kuwa na mamlaka,” alisema Nyambu.

Aidha, aliwalaumu mawakili kwa kuchukua muda mrefu kujadili kesi mahakamani, na kupendekeza mahakama kupokea lalama moja kwa moja kutoka kwa wakazi na kuzuru mashinani kutatua kesi ya ardhi kama ilivyokuwa hapo awali ili kupunguza kukawia kwa kesi za ardhi.

“Mawakili wamechangia shida nyingi katika kesi za ardhi kwa sababu huchukua kesi na stakabadhi nyingi zinazochelewesha kutatuliwa kwa kesi ya ardhi na mahakimu. Tunapendekeza mahakimu wawe wakizuru mashinani na kutatua kesi hizo,” aliongeza Nyambu.

Mizozo ya ardhi katika ukanda wa Pwani imekuwa donda sugu hata baada ya wanaharakati wa kutetea maswala ya ardhi kuwashinikiza viongozi kupitisha sheria maalum bungeni ya kutatua mizozo ya ardhi kwa usawa na uwazi na kwa kutoa vyeti vya hati miliki za ardhi kwa wakenya.