Wananchi katoka eneo la Nyakach wametakiwa kuzingatia sheria za ujenzi na nyumba wanapojenga nyumba zao.
Hii ni kutaka kuboresha makazi pamoja na kudhibiti majanga ya nyumba kuporomoka kutokana na utaratibu mbaya unaotumiwa mara nyingi wakati wa ujenzi.
Mkaguzi wa ubora wa mijengo tawi la Kisumu, Raymond Nyakuti aliwataka wakazi kuhakikisha kwamba wanatumia wataalamu kupima eneo wanalonuia kuweka mjengo wowote na pia kuhakikisha uchoraji wa ramani ya mjengo wowote kabla ya ujenzi wowote kuanzishwa.
''Tumekuwa na visa vya majumba kuporomoka hata kabla ya kumalizika kujengwa, hali ambayo imeendelea kusababisha maafa na hasara kwa wananchi,'' alisema Nyakuti siku ya Jumamosi.
Aidha, afisa huyo aliwaonya wananchi dhidi ya kutumia wataalamu bandia kusimamia ujenzi wa nyumba zao. Alisema kuwa nyumba za makazi, hasa katika maeneo ya miji zinataka uzingatiaji wa mambo mengi ikiwemo ubora wa vifaa vya ujenzi.
Haya yanajiri wakati kunaendelea kuripotiwa visa vya mijengo kuporomoka kwenye maeneo mengi nchini.