Wanaopenda kuzuru maeneo ya shule nyakati za likizo wameonywa dhidi ya kusababisha madhara katika shule.
Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Makora kwenye Kaunti Ndogo ya Kisumu East, Samson Okoth, ametoa ilani kwa wakazi ambao hutembelea maeneo ya shule nyakati za likizo ili kubarizi.
Okoth amesema wanaozuru shule nyakati za likizo hutumia maeneo yake kwa burudani. Mwalimu mkuu huyo amesema kuwa wasipokoma, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Akiongea kwenye mkutano wa naibu wa chifu eneo hilo ambao uliandaliwa siku ya Alhamisi kwa madhumuni ya kudhibiti usalama, Okoth alihoji kuwa watu hao wamesababisha madhara mengi yenye gharama za juu kwenye shule za eneo hilo, wakati vifaa vya shule vikipotea huku mali nyingi ikiharibiwa.
''Mara nyingi madirisha ya madarasa shuleni huvunjwa na vio kupasuliwa kwa kurushiwa mawe na vijana ambao huzuru maeneo ya shule hizo kwa michezo,'' alisema Okoth.
Caleb Thuogo ambaye ni mkazi eneo hilo alidokeza kuwa watu wengine hulisha mifugo wao shuleni na mara kuingia na kuvunja madawati kwenye madarasa.