Agizo limetolewa kwa wanunuzi na wauzaji wa malighafi katika Kaunti Ndogo ya Kisumu Magharibi kukoma kupeleka biashara hiyo shuleni.
Inasemekana kuwa wafanyibiashara hao hulenga shule za msingi kupitia kwa wanafunzi ili kukusanya bidhaa hizo. Agizo hilo limetokea baada ya wazazi kulalamikia hali ambayo wanao ambao ni wanafunzi kwenye shule za eneo hilo kuonekana kuingilia biashara hiyo badala ya kuzingatia masomo.
Wazazi na walimu kwa pamoja walijadili kukomesha hali hiyo shuleni walipotuma ujumbe kwa wafanyibiashara hao wakiwataka kulenge kwingine kunogesha biashara yao na wala siyo shuleni tena.
Katika Shule ya Msingi ya Riat, walimu walikutana na wazazi mnamo siku ya Jumatano na kujadili swala hilo kabla ya kutoa tangazo kwa wanafunzi baada ya kikao.
''Kuanzia leo tumepiga marufuku biashara ya malighafi shuleni. Tunataka wanafunzi kuzingatia masomo ambayo ni muhimu kwa maisha yao ya baadaye,'' alisema naibu wa mwalimu mkuu wa shule hiyo Emlly Mwanda.
Baadhi ya wazazi walidokeza kuwa wanao hushinda wakisaka bidhaa hizo mitaani, hali ambayo wanahofia itachangia uhuni miongoni mwa wanafunzi, ikizingatiwa kuwa wameanza kuzoea kushika pesa mapema.
Pia walisema kuwa hali hiyo imechangia wizi wa vifaa vya chuma kijijini ambavyo hunyakuliwa na kuuziwa wafanyibiashara hao kama malighafi.