Siku moja tu baada ya Waandishi wa habari kuangazia suala la biashara ya malighafi iliyopigwa marufuku kwenye baadhi ya shule za msingi katika eneo la Kisumu Magharibi, mmoja wa wanaofanya kazi hiyo amejitokeza kuitetea.
Mapema mnamo siku ya Alhamisi, wazazi pamoja na walimu katika Shule ya Msingi ya Riat waliwataka wafanyibiashara hao kukoma kuyatumia wanafunzi katika kukusanya vyuma kuu kuu ili kuwauzia.
Wensealous Opiyo kutoka eneo hilo amewaambia Waandishi wa habari kuwa jambo hilo lisieleweke vibaya miongoni mwa wazazi na walimu, akitaka wenzake kubadilisha mbinu ya kununua bidhaa hizo kutoka kwa wakazi.
Opiyo alisema hiyo ni mojawapo ya njia za kuwapa wazazi hela na kupiga jeki gharama za masomo kwa wanao.
''Kile tunastahili kufanya ni kuzuia kuwapa wanafunzi pesa mkononi na badala kuwabadilishia vifaa vya masomo kama vile, kalamu na vitabu miongoni mwa bidhaa nyinginezo za masomo,'' alisema Opiyo.
Alidokeza kuwa vyuma kuu kuu vimetapakaa vijijini na havina kazi ila kukusanywa na kuuzia kampuni za kutengeza vyuma na mabati pamoja na bidhaa nyinginezo zinazotokana na malighafi haayo.
Opiyo pia alidokeza kuwa biashara hiyo ni mojawapo ya njia za kuzidisha nafasi za ajira kwa vijana na kuimarisha uchumi wa taifa, huku ikiwa mojawapo ya njia za kuboresha mazingira katika maeneo, ikizingatiwa kuwa baadhi ya vyuma kuu kuu husalia ardhini kwa muda mrefu na kuwa hatari katika mazingira.
Aliongezea kwamba wanalenga wanafunzi na kutegemea shule kwa kuwa wao hutoka kila pembe kwa hiyo huwa rahisi kwao kukusanya bidhaa hizo maradufu.