Wanasiasa wawili wameahidi kuunga mkono chama cha walimu cha Knut katika mgomo wao kufuatia kutolipwa kwa nyongeza yao ya mshahara.
Wakiongea katika eneo la Masimba, Masaba Kusini, Kaunti ya Kisii, siku ya Ijumaa, wanasiasa hao walisema wako tayari kwa yote yale ili kuhakikisha haki za walimu zimetimizwa na serikali kuu.
Benard Moseti alisema kuwa walimu wamekumbwa na umasikini nchini licha ya kuwa wao ndio huleta elimu kwa wale wanaowanyima haki zao.
Aidha, alisema yeye kama mwanasiasa hataleta siasa za Kenya katika maswala ya kupigania haki za walimu.
Nyamoko alisema tawi la Knut la Masaba Kusini ambalo laongozwa na Meshack Aiko limpigie kura wakati wa uchaguzi ujao ili akifika bungeni aweze kutetea maswala ya unyanyasaji wa haki za walimu.
“Mkisimama nami katika uchaguzi wa 2017 nitahakikisha niko bungeni kama mjumbe wenu wa Nyaribari Masaba nikitetea haki za walimu kikamilifu. Nitahakikisha pia mazingira ya kufanya kazi kwa walimu yatakuwa mazuri ya kufana,” alisema Moseti.
Ocharo Kebira pia aliwahakikishia walimu mkono wake katika maswala ya haki zao akidai atawatetea walimu wapate haki zao hata kwa sasa ili awaonyeshe kuwa yeye ni kiongozi.
“Mimi niko na walimu na nasimama nanyi ili mwaka wa 2017 tukienda uchaguzi, mjue mimi ni kiongozi wenu wa vitendo,” alisema Ocharo.