Wanawake katika ukanda wa Pwani wamehimizwa kuzidi kuendeleza hamasa mashinani kuhusu maswala ya misimamo mikali miongoni mwa vijana ili kuimarisha usalama.
Kulingana na Naibu Mwenyekiti wa chama cha maendeleo ya Wanawake nchini Bi Sureya Hersi, kutokana na idadi kubwa ya vijana wadogo kujitosa katika maswala ya misimamo mikali na kuzua hofu ya ukosefu wa usalama kwa jamii, ni lazima kwa swala hilo kuangaziwa.
Akizungumza katika kongamano la wanawake mjini Mombasa siku ya Jumapili, Sureya alisema kwamba hamasa hiyo ikiendelezwa mashinani, basi vijana wengi watanusurika na hali hiyo na usalama wa eneo la Pwani utaimarika.
“Wanawake tujitokeza na kuzidi kuendelea na hamasa mashinani ili kuwanusuru vijana wetu waliyojitosa katika maswala ya misimamo mikali ili kuona kwamba eneo letu la Pwani liko salama. Hatua hii itatusadia pakubwa kubadilisha fikra mbaya za vijana wetu,” alisema Sureya.
Aidha, aliwashikiza viongozi wa kisiasa na wale wa kidini kuunga mkono juhudi za akina mama mashinani katika kampeni hiyo ya kuwanasua vijana na kuimarisha usalama.
Wakati uo huo kiongozi huyo wa wanawake aliahidi kuungana na akina mama mashinani na kuendelea kampeni hiyo ya hamasa ili kuona kwamba vijana waliyojiunga na makundi ya kihalifu wanajisalimisha.