Wanawake watatu ambao walinaswa siku ya Jumatano wakiwa na vifaa zinazoshukiwa kuwa za ugaidi katika mji wa Mtwapa, watakaa kizuizini kwa siku thelathini zijazo huku wakisubiri uchunguzi kutoka idara ya polisi.
Washukiwa hao walishikwa katika eneo la kupima magari uzani katika mji wa Mtwapa ambapo inadaiwa walikuwa njiani kwenye safari kuenda eneo la kaskazini mwa Kenya.
Kulingana na uamuzi uliotolewa siku ya Alhamisi na hakimu mkuu wa Mahakama Makuu ya Mombasa, Diana Mochache, watuhumiwa hao watakaa kizuizini kwa muda huo ili msimamizi mkuu wa kesi hiyo apate muda wa kutosha wa kufanya utafiti wa kutosha kuhusiana na vifaa hivyo vilivyopatikana na washukiwa hao.
Kulingana na mchunguzi wa kesi hiyo Yvonne Mulobi, washukiwa hao watahitajika kujibu tuhuma za kuwa washirika wa kundi haramu la al-Shaabab.
Mulobi alisema kuwa washukiwa hao watasaidia upande wa kufanya uchunguzi kupata habari muhimu kuhusiana na makundi ya kigaidi.
Aidha, mchunguzi huyo alisema kuwa washukiwa hao walipatikana na vifaa vya mawasilianao kama tarakilishi, simu za rununu, pamoja na viatu vinavyotumiwa na wanajeshi.
Washukiwa hao walishikwa siku chache baada ya serikali ya Kenya kuanza kuwafurusha washukiwa wa ugaidi katika eneo la Lamu kwenye msitu wa Boni, ambapo wanajeshi wa KDF wanaongoza operesheni hiyo.