Share news tips with us here at Hivisasa

Polisi kutoka eneo la Tala wamewatia mbaroni washukiwa wawili wanaodaiwa kumwibia mwanamke mmoja Sh23,000, baada ya kumlaghai kuwa wanamwombea.

Inadaiwa kuwa watu hao, mwanamume mmoja na mwanamke, waliingia katika duka moja walipomhadaa mwenye duka hilo kuwa wanataka kumwombea na kisha kumwibia pesa zake.

Akidhibitisha kisa hicho, naibu wa chifu wa Tala Francis Mulinge alisema kuwa visa hivyo vimekuwa vikishuhudiwa mno katika Soko hilo la Tala, hasa siku za Soko.

"Watu hawa huja wakati wa soko kwa kuwa watu huwa wamefurika mno sokoni na kuwahadaa watu kuwa watawaombea na kisha kuwaibia bila ya wao kujua,” alisema Mulinge.

Chifu huyo aliwasuta watu wenye nia ya kutaka kutajirika kwa urahisi kwa kutumia njia zisizo halali na kuwashauri kutumia jasho lao.

Vilevile, Mulinge alisema kuwa mkono wa sheria utawafunza watu wenye malengo mabaya kama hayo.

"Watu hupenda kuvuna wasipopanda. Cha kushangaza ni kuwa wanatumia njia zisizo halali,lakini mkono wa sheria utapambana nao vilivyo,” alisema Mulinge.

Aliwaomba wakazi wa eneo hilo kuwa waangalifu na kuripoti watu wanaowashuku kuwa na nia ya kuwalaghai.

Washukiwa hao wanazuiliwa katika Kituo cha polisi cha Tala huku uchunguzi ukiendelea.