Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Washukiwa wawili wa ulaghai  wametiwa mbaroni katika soko la kikuyu wakiwahadaa wananchi kwa kuwauzia simu bandia.

Akidhibitisha kisa hicho siku ya Alhamisi, mkuu wa polisi katika eneo la Kikuyu Mutune Maweu alisema kwamba ulaghai ulikuwa umekita mizizi eneo la sokoni kwa muda wa miezi miwili sasa.

Alisema zaidi ya watu wanne walikuwa wameripoti visa vya kulaghaiwa pesa zao.

Maweu alisema kwamba walaghai hao walikuwa wanatumia mbinu za kutoshukiwa na yeyote ili kutekeleza uhalifu wao.

Alisema walikuwa wanavalia suti na mara nyingi walijifanya wamepotea ili kuulizia njia kwa wananchi.

Mkuu wa polisi alisema walaghai hao walitumia mafuta ambayo polisi wanashuku ni dawa wanayotumia kumpumbaza wananchi ili wasiweze kufikiria kawaida.

Alisema wale waliohadaiwa walikuwa hawaelewi jinsi walivyowafuata watu wale kisha kunyang'anywa bidhaa zao.

Alisema polisi walipashwa habari na mchuuzi mmoja aliyekuwa sokoni na inadaiwa kuwa waalifu hao walikuwa wanatekeleza uovu huo katika soko tofauti na walikuwa na siku maalum ya kila soko.

"Polisi waliwakamata wawili hao na kuwakagua na kupata mafuta hayo ambayo yanashukiwa ni ya kutekeleza ualifu huu na simu za rununu mbili. Moja ya kweli na inayofanya kazi na nyingine ni bandia bali ni kama simu lakini ndani ni udongo,” alisema Maweu.

Alisema kuwa wale wanaosimamia soko wanapaswa kushirikiana na maafisa wa usalama kwa kurepoti visa vya aina hii ili kuweza kukabiliana na swala hilo.