Washukiwa wanne wa ugaidi wa asili ya Somalia walitiwa mbaroni siku ya Ijumaa katika nyumba moja waliokuwa wameishi kwa siku nne.
Wanne hao walihamia katika ploti moja ya kukodisha katika eneo la Banana na polisi wanashuku kuwa wanne hao walikuwa na njama ya kutekeleza maovu hivi karibuni.
Polisi pia waliweza kunasa mashini za tarakilishi ambazo wanashuku zinaweza wasaidia kwa uchunguzi, na pia bunduki mbili za aina ya AK 47 na risasi 52.
Wanne hao pia walikuwa na stakabadhi bandia za kuwa Kenya.
Akidhibitisha kisa hicho, Ofisa mkuu katika kaunti ndogo ya Kiambu Stephen Ng'etich alisema kuwa wanne hao walinaswa mapema leo kwa usaidizi wa mwenye nyumba hizo.
Alisema kuwa mwenye ploti hiyo alifuata mtindo wa kuitisha stakabadhi ya wapangaji wake lakini walizozitoa wanne hao zilikuwa bandia.
Ng'etich alisema kuwa mwenye nyumba hizo aliripoti kisa hicho katika Kituo cha Polisi cha Banana na polisi wakachukuwa hatua.
Alisema kuwa wanne hao walitiwa mbaroni na walifikishwa katika Kituo cha Polisi cha Kiambu ambako uchunguzi zaidi unaendelea.
“Nawahimiza wenye nyumba za kukodisha kuiga mfano huu kwa kutaka kujua wapangaji ili wasiwe magaidi ambao wanataka kuangamiza nchi yetu. Wananchi na hasusan vyama vya Nyumba Kumi vinafaa kuwa katika mstari wa mbele kutambua watu wa aina hii," alisema Ng'etich.
Hata hivyo, alisema kuwa wanne hao watafikishwa mahakamani siku ya Jumatatu baada ya polisi kufanya uchunguzi wao.