Share news tips with us here at Hivisasa

Maafisa wa polisi wamewatia mbaroni washukiwa wawili wa uhalifu wakiwa na sare za wanajeshi katika mji wa Kebirigo, wilayani Nyamira.

Washukiwa hao walitiwa mbaroni na maafisa wa polisi wa kituo cha Kebirigo siku ya Jumanne, wakiwa na sare hizo kinyume na sheria, baada ya kupokezwa habari kutoka kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Nyamira, mkuu wa wa polisi wilayani Ricah Ongare alisema washukiwa hao walikuwa wakitembea katika mji wa Kebirigo, kabla ya kushukiwa na wananchi ambao walipiga ripoti kwa maafisa wa polisi.

Kulingana na mkuu huyo wa polisi, washukiwa hao walikuwa na bunduki ya kujitengenezea, pamoja na sare hizo za maafisa wa polisi.

Aidha, mkuu wa polisi huyo alipongeza wananchi kwa kupasha habari kwa maafisa wa polisi, na kuwaomba wananchi kuendelea kuwa macho.

“Wananchi ndio walisaidia kukamatwa kwa washukiwa hawa wawili kwani ndio waliwashuku na kupiga ripoti kwa polisi kisha polisi wakawatia mbaroni,” alisema Ongare.

Hii si mara ya kwanza washukiwa wa uhalifu kutiwa mbaroni katika kaunti ya Nyamira, ikikumbukwa kwa miezi miwili iliyopita washukiwa kadhaa walitiwa mbaroni.

Washukiwa hao walipelekwa hadi kituo cha polisi cha Nyamira na watafikishwa mahakamani pindi tu uchunguzi utakapokamilika.