Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Takriban wasichana elfu nane wameepushwa na swala la ukeketaji kuanzia mwaka wa 2005 hadi sasa, baada ya kupitia mpango wa kutoa mafunzo kwa waliobaleghe unaoendelezwa na parokia ya kanisa katoliki ya St Francis Lare kaunti ya Nakuru.

Thibitisho hilo limetolewa na mwenyekiti wa muungano wa akina mama wakatoliki wa Catholic Women Association kwenye parokia hiyo Mary Nyokabi, aliyesema mpango huo ulianzishwa kutokana na tamaduni ya ukeketaji ambayo ilikuwa imekidhiri katika eneo hilo.

Nyokabi, kupitia kwa mahojiano na wanahabari siku ya Jumatatu alisema mafunzo hayo hujumuisha wasichana walio na umri wa miaka 12 hadi miaka 18, na baadhi ya yale mambo wasichana hao hufunzwa ni changamoto ambazo wasichana hupitia wanapobaleghe.

"Wasichana wetu wengi walikuwa wanakeketwa kwa miaka iliyopita lakini mnamo mwaka wa 2005, kuna watu walioanza mradi wa kupinga ukeketaji. Mtawa mmoja kwa jina la Ephijinia alitufadhili na tukaweza kuwakusanya wasichana na tukaanza kuwapa mafunzo yanayohusu kubaleghe badala yao kukeketwa. Kutoka huo mwaka wa 2005 tumekuwa tukiandaa semina na kufikia sasa wasichana elfu nane wamepitia mpango huu," alisema mwenyekiti huyo.

Ni mafunzo anayosema yameanza kuzaa matunda na ambayo pia kwa wakati mwingine hujumuisha wazazi ambao hufahamishwa kuhusiana na madhara ya ukeketaji .

Wito wake ni kwa wale wanaoendeleza tamaduni hiyo kukoma, huku akisema tamaduni hiyo imeharamishwa kisheria na badala yake, amewataka wazazi hao kuhakikisha kwamba watoto wao wa kike wanapata mafunzo hayo anayoyataja kama yenye manufaa.

"Tayari tumeona matunda, na isitoshe, tumewaelimisha wazazi wao kuhusiana na madhara ya kuwakeketa wasichana wao. Tunaendelea kuhimiza wasichana wasikeketwe na wachache wanaojificha na kuwakeketa wasichana wao tunawaamia ukeketeaji ni kinyume cha sheria," aliongezea.

"Waleteni katika semina tuwafunze ili waweze kujua yaliyo mbele yao. Zamani wasichana wengi walikuwa wanapata mimba wakiwa shuleni lakini tunaona mambo hayo yamepungua," aliongeza Nyokabi.

Amefichua kuwa mradi huo wa kutoa mafunzo utaendelezwa mwezi Desemba mwaka huu katika kanisa hilo, huku akiwataka pia wafadhili kujitokeza kufanikisha mradi huo.

"Mwaka huu wa 2015 tutakuwa na semina ya wasichana Desemba. Hata hivyo, semina hiyo mara nyingi hudumu kwa siku nne. Tuna changamoto nyingi kwa sababu ya kiangazi, na hivyo tunawahimiza wafadhili watuchangie fedha kidogo kwa sasabu wanahitaji kula vizuri na pia kuna walimu walio na ujuzi kuhusiana na jinsi wasichana wanavyokuwa," aliongeza mwenyekiti huyo.