Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wataalam wanaounga mkono uzalishaji chakula kupitia kwa mbinu ya kisayansi ya GMO wamewataka wanasiasa kuondoa siasa katika mjadala huo.

Wakihutubia wakulima mjini Eldoret siku ya Ijumaa, wataalam hao walisema wanasiasa wanatumia swala hilo kujipatia umaarufu badala ya kuelezea wakulima ukweli kuhusu GMO.

Mtafiti kuhusu uzalishaji chakula kupitia kwa mbinu za kisayansi katika chuo kikuu cha Nairobi Dkt Joel Ochieng alisema mjadala kuhusu uzalishaji huo umechukua mkondo wa kisiasa badala ya wanasayansi kuachiwa nafasi ya kuelezea Wakenya manufaa ya GMO.

“Iwapo Wakenya watakumbatia uzalishaji chakula kupitia kwa mbinu hii, viwango vya uzalishaji chakula nchini vitaimarika hivyo basi kutakuwa na usalama wa chakula,” alisema Ochieng.

Wataalam hao walipuuzilia mbali dhana kwamba vyakula ambavyo huzalishwa kupitia kwa GMO ni hatari kwa afya ya binadamu.

Dkt Ochieng alisema mataifa mengi kote ulimwenguni yanatumia vyakula hivyo kutengeneza dawa mbalimbali ambazo zimekubalika na mashirika ya kimataifa hivyo basi dhana kwamba GMO husababisha magonjwa ni potovu.

Mtaalam huyo alisema kuwa vyakula vilivyozalishwa kupitia kwa GMO vimedhibitishwa kuwa na uwezo wa kupunguza aina mbalimbali ya saratani.

Licha ya tetesi za wataalam hao, wakulima kutoka North-Rift bado hawaja kubali mbinu hiyo kwa madai kuwa ina athari za kiafya.

Hivi maajuzi wakulima hao walishiirki maandamano ya kupinga uzalishaji chakula kupitia kwa mbinu hiyo ya kisayansi.