Watu watatu walipata majeraha siku ya Jumatatu baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuhusika kwenye ajali, nje ya duka kuu la bidhaa la Uchumi mjini Kisii.
Gari hilo ambalo lilikuwa linatoka mji wa Keroka kuelekea mji wa Kisii linasemekana lilipoteza mwelekeo wakati dereva wake alipokuwa akijaribu kuligeuza ili kuingia katika kituo cha magari ambapo aliepa kuligonga lori la mchanga lililokuwa limeegeshwa kando ya barabara na kuanguka kwenye mtaro.
Kulingana na Dan Mose ambaye alishuhudia ajali hiyo, gari hilo la Matatu aina ya Nissan lilitoka kwa mwendo wa kasi kutoka sehemu ya Keroka ambapo dereva huyo alishindwa kulidhibiti na kupotoka barabarani na kuangukia shimo lilo karibu la kupitisha maji.
Mose alisema kuwa gari hilo lilikuwa na abiria wengi lakini watatu ndio waliojeruhiwa kwa kukatwakatwa na vioo vya madirisha ya gari hilo.
Hata hivyo, dereva na utingo waliepuka na majeraha madogo huku watatu hao wakipelekwa katika hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii.
Kiongozi mmoja kutoka sehemu hiyo ya Nyankongo, Charles Moseti, aliwataka madereva kuwa makini kila mara wanapokuwa barabarani ikizingatiwa kuwa mvua nyingi katika mji huo na eneo la Gusii imeanza kushuhudiwa.