Wavuvi wa kutumia motaboti na mashua za kuendeshwa na makasia wamelalamikia kudhulumiwa na maafisa wa polisi wa halmashauri ya kukusanya ushuru nchini.
Inasemekana maafisa hao wamekuwa wakiwashika na kuwanyang'anya vyombo vyao na kuvizuilia na kutaka kupewa hela ili waviachilie.
Wavuvi hao wakiongea siku ya Jumanne katika ufuo wa DeepSea kupitia kwa kiongozi wao Rashid Mwinyi, baadhi ya mafisaa wa halmashauri ya ushuru wamekuwa na mazoea ya kuwaomba hela ndipo wawaache kuendelea kuvua kwenye Bahari Indi suala ambalo alisema ni haramu na kinyume na sheria.
"Wavuvi hulipa ushuru kama walipa kodi wengine kwa hivyo si haki kamwe kuombwa kutoa hela kila mara ndio tuendelee na uvuvi. Sisi hatujawahi kukosa kulipa ada hiyo kwa serikali," alidai Mwinyi.
Mwinyi alisema kuwa juhudi za kuripoti visa hivyo kwenye idara husika hazijazaa matunda kwani husikilizwa na kuahidiwa kuwa watashughulikiwa lakini dhuluma hiyo huendelea siku chache baadaye.
Wavuvi hao walimwomba gavana wa Mombasa Hassan Joho kwa ushirikiano na serikali ya taifa kupigana na ufisadi unaoendelezwa na maafisa wa ushuru kwenye bandari na hasa baharini.