Wakazi wa kaunti ya kisii wamewaomba wawakilishi wote wa wadi katika kaunti ya kisii kuungana pamoja kwa ushirikiano kutafuta mbinu ya kuinua viwango vya elimu katika shule zote zilizomo katika kaunti hiyo.
Wakiongea na waandishi wa habari siku ya Jumatatau katika mji wa kisii, wakazi hao waliomba wawakilishi wote wa kaunti hiyo kutafuta njia ya kuinua viwango vya elimu katika shule za msingi na za upili huku wakisema viwango wa elimu vimeonekana kudorora katika kaunti hiyo.
“Wawakilishi wanapaswa kujiunga pamoja waanze kuzitembelea shule ili kuona jinsi elimu ilivyo na jinsi inavyoendeshwa. Wakipata viwango vya elimu viko chini na wanunulie shule hizo vitabu vya kusoma shule za kisii zitakuwa zimeinuka zaidi kimasomo,” alisema John Ondara, mkazi.
Wakati huo huo, wakaazi hao walisema kuwa kwa takribani miaka mitatu iliyopita, shule za msingi katika eneo hilo hazikuwa zikifanya vyema katika mitihani ya kitaifa jambo ambalo liliwalazimu kuomba wawakilishi wa wadi kutafuta mbinu ya kuinua viwango vya elimu.
“Ikiwa kuna upungufu wa walimu katika shule zetu, wawakilishi wanapaswa kuomba serikali iongeze walimu au waajiri walimu wengine wale wa kulipwa na wazazi ili kuinua viwango vya elimu katika shule za kisii,” alisema Victor Nyanuri, mkazi.
Wakazi wengine nao waliweza kupendekeza kuwa sekta ya elimu yastahili kuwa chini ya uongonzi wa serikali ya kaunti huku wakidai kuwa serikali ya kitaifa inafeli haswa kwa kutowaongeza mshahara walimu jinsi wanavyohitaji, jambo ambalo pia walisema linasababisha kudorora kwa masomo katika shule.
“Tunaomba sekta ya elimu iwekwe chini ya uongonzi wa kaunti maana tunaona serikali kuu ndio husababisha masomo kudorora kwa kutowaongeza walimu mshahara. Shule zingekua chini ya usimamizi wa serikali ya kaunti mambo haya hayangeshuhudiwa kamwe,” alisema Eunice Nyakundi, mkazi.