Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wazazi wametakiwa kutulia manyumbani mwao na wanao walio na umri usiozidi miaka mitano ili kuwapa madakitari wanaopeana chanjo ya polio kazi rahisi. 

Akizungumza katika kanisa la Legion Maria la Nyakoko, siku ya Jumapili, afisa anayesimamia shughuli hiyo katika lokesheni ya Nyakoko, iliyoko Kaunti Ndogo ya Muhoroni, Hezron Loinen, aliwataka wazazi kuelewa kuwa chanjo inayopeanwa haina madhara yoyote kwa watoto.

''Tuna himiza wazazi kutafuta fursa ya kuhakikisha kwamba wanao wamepata chanjo kabla ya kumalizika kwa kipindi kinachotarajiwa,'' alisema Loinen. 

Katika maeneo mengine ya eneo hilo, shughuli za chanjo ziliendelea taratibu siku ya Jumatatu huku madakitari wakichukuwa nafasi ya kuwadokezea umuhimu wa chanjo hiyo kabla kutekeleza kuwachanja watoto. 

Dk Roseline Apiyo aliwashukuru wazazi kwa kuwa wamakinifu na kuitikia huduma za madakitari bila pingamizi.

"Afya ya watoto wenu haihitaji pingamizi zozote. Serikali imetuhakikishia kuwa chanjo hii haina madhara yoyote,'' alisema Apiyo. 

Aidha, wakazi waliofuga mbwa wametakiwa kuwafunga mbwa hao ili kuepuka visa vya madakitari kushambuliwa na mbwa hao kama ilivyokuwa msimu uliopita ambapo visa kama hivyo viliripotiwa.