Mkurugenzi mkuu wa elimu katika Kaunti ya Kisii Richard Chepkawai amewataka walezi na wazazi wa kambo wanao jukumu la kulea watoto mayatima kuwalea watoto hao kama wanao bila kuwatesa.
Visa vya dhuluma kwa mayatima vimekuwa vikishuhudiwa na kuripotiwa katika sehemu na idara tofauti za elimu na zile zinashughulikia masuala ya watoto nchini.
Afisa huyo wa elimu alisema haya siku ya Jumanne katika ofisi yake siku chache baada ya kijana mmoja kuwatembelea kutafuta msaada katika ofisi yake wiki jana kufuatia madai ya kuwa alikuwa ananyanyaswa kule alikokuwa akilelewa na wazazi wa kambo ambao alidai walidinda kumpa haki yake ya kuenda shuleni.
Aidha, afisa Chepkawai aliwataka wazazi hao wenye tabia hiyo kukoma kuwanyanyasa mayatima wanapojitwika mzigo kama huo wa kuwalea watoto hao, hali ambayo alisema huwapelekea mayatima kutoweka kuhamia miji mikuu ambapo wanajipata kuwa chokoraa.
Mkurugenzi huyo vile vile, aliwashauri watoto mayatima kufuata utaratibu ufaao wanapojipata kwenye hali hiyo ya dhuluma na kuwataka kutembelea ofisi za mkuu wa wilaya kutoa ripoti zao na kufuatiliziwa kutoka hapo iwapo wanadhulumiwa na wazazi wao wa kambo badala ya kuenda moja kwa moja hadi ofisini mwake.
“Iwapo kuna mtoto yeyote anayedhulumiwa atembelee katika ofisi ya wilaya yao husika ili kupata usaidizi kutoka kwa maafisa wa wilaya,” alishauri mkurugenzi Chepkawai.