Wazazi kutoka Kaunti ya Kisii wameonywa dhidi ya kutengana wanapobarikiwa na mtoto mlemavu katika familia zao.
Akiongea siku ya Jumatano katika hafla ya kuwasaidia watoto zeruzeru na miwani zilizotolewa na wahisani wema iliyoandaliwa katika ukumbi wa michezo na utamaduni mjini Kisii, mkuu wa idara ya michezo na utamaduni katika Kaunti ya Kisii Ibrahim Moiro Omari aliwaomba wazazi wanaotabia kama hiyo kukoma kwani sio kwa uwezo wao kupata watoto hao na kuwaambia kuwa watoto hao ni baraka kubwa kwao.
Aidha, aliwahimiza wazazi kuwa ni wajibu wao kumkubali na kushirikiana kama familia moja wanapobarikiwa na watoto kama hao ili watoto hao pia waweze kujiendeleza kimaisha haswa kimasomo.
Kwa mujibu wa Omari, kuna familia nyingi ambazo zimetengana kutokana na kupata mtoto mlemavu katika jamii yao akiongeza kuwa akina mama ndio mara nyingi hubeba mzigo huo na kusumbuka kwa kukosa ushirikiano na mume zao.
“Nawaomba wazazi kuwa wakati mtoto mlemavu amezaliwa katika familia isiwe ni utengano bali wawakubali katika familia na kumtunza kama watoto wengine,” alihoji Omari.
Kwingineko alisema kuwa idara yake ipo tayari kila wakati kushirikiana na wanaoishi na ulemavu kuhakikisha wamepata haki zao kama wakenya wengine.
“Mlango wa Idara yangu huwazi kwa wanaoishi na ulemavu ambao anahitaji usaidizi na nahimiza yeyote anayeshida kufika na kuwasilisha malalamishi yake ili aweze kushughulikiwa kikamilifu,” aliongezea Omari.
Pia aliipongeza serikali ya Kaunti ya Kisii kwa kuwajali wanaoishi na ulemavu na kuiomba kuendelea kuwasaidia kila kuchao ili nao waweze kupata elimu na vitu vingine kama wananchi wengine.