Afisa wa mauzo katika Chuo Kikuu cha Kisii Zachary Mose amewaomba wazazi katika Kaunti ya Kisii kuwapeleka wanao shuleni ili kupata elimu ambayo itawasaidia siku zijazo.
kulingana na afisa huyo, zawadi ya kipekee ambayo mzazi atamwanchia mtoto wake kama uridhi ni elimu bali si pesa.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumapili mjini Kisii, afisa huyo alisema kila mzazi anastahili kuhakikisha mtoto wake amepata masomo maana elimu ndio msingi wa maisha kwa binadamu.
“Wazazi katika Kaunti ya Kisii wanafaa kuruhusu watoto kupata Elimu ambayo ni ya manufaa maishani. Mtoto yeyote ambaye hukosa kuelimika darasani huwa na vikwazo vingi maishani mwake ikiwemo kukosa ajira na hata kuheshimika katika Jamii, alisema Mose.
Afisa huyo pia alisema umuhimu wa mtoto kupata masomo ni kupata kazi ya kufanya nchini huku akisema watoto wengi ambao walikosa kupelekwa shuleni na wazazi wao wameishia kuwa vijana wa kurandaranda mitaani jambo ambalo huchangia umaskini katika jamii.
Aidha, aliwaonya wazazi wanaowatumia watoto wao kufanya kazi za sulubu manyumbani huku akisema kuwa hiyo ni kumuumiza mtoto na kumnyima haki ya masomo.
“Naomba kila mzazi kuhakikisha mtoto wake yuaenda shuleni ili kupata mafinzo kutoka kwa walimu ili waje kujisaidia siku za usoni,” aliongezea Mose.