Wazazi kutoka kaunti ya Nyamira wameiomba serikali ya kitaifa na tume ya kuwaajiri walimu kuwashughulikia walimu ili kuzuia mgomo wa chama cha Kuppet ambao chama hicho kimeapa kufanya muhula ujao kama matakwa yao hayataafikiwa.
Wakiongea hii leo, Ijumaa na mwaandishi huyu katika sehemu ya Matutu wadi ya Gesima, wazazi hao wakiongozwa na mwenyekiti wa Shule ya Msingi ya Matutu George Onsare, waliiomba serikali kuwashughulikia walimu ili kuzuia migomo ambayo inashuhudiwa kila mara.
Kulingana na wazazi hao, walimu wakigoma haswa katika muhula wa tatu, wanafunzi ndio hukumbwa na shida kubwa kwa sababu muhula huo ndio mithiani wa kitaifa huandaliwa.
Tabitha Mocheche, mmoja wa wazazi hao alisema kuwa walimu wanastahilii kushughulikiwa kwani wanafanya kazi ngumu na njia ya kuzuia migomo hiyo ni kushirikiana na kupata suluhu la kudumu katika sekta ya elimu
“Naomba serikali yetu na tume ya kuwaajiri walimu kuwashughulikia na kuelewana nao ili mambo ya mgomo ambayo sisi hutuumiza sisi kama wazazi na wana wetu,” alihoji Mocheche.
Onsare aliongezea kusema kuwa wakati walimu wanagoma, viwango vya masomo huadhiriea kwa asilimia kubwa, na wanafunzi huwa na shida kubwa haswa wanaofanya mitihani wa kitaifa.