Wazazi kutoka Kaunti ya Kisii wameombwa kujitolea na kushirikiana na walimu ili kuinua viwango vya masomo.
Akiongea siku ya Ijumaa katika shule ya upili ya wasichana ya Nyabururu ilioko eneo bunge la Kitutu Chache Kaunti ya Kisii, katika hafla ya siku ya elimu, mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Elimu, Erastus Muthuuri Kiugu, aliwaomba wazazi kushirikiana na walimu ili viwango vya masomo vinawiri katika kaunti ya kisii.
"Nawaomba wazazi wote kushirikiana na walimu kama njia moja ya kuinua viwango vya elimu," alisema Kiugu.
Aidha, alisema kuwa sekta ya elimu inastahili kupewa nafasi ya kwanza katika jamii.
"Sekta ya elimu inastahili kupewa nafasi ya kwanza kwa kuwa ndio msingi wa kila jambo na kazi mtu anayofanya,"aliongezea Kiugu.
Aliwahimiza walimu kujitolea wanapowafunza wanafunzi ili shule za Kisii ziweze kuzoa alama bora kila wakati na kuwezesha wanafunzi hao kuitimisha ndoto zao.