Naibu mwenyekiti wa mashindano ya tamasha za muziki katika shule za msingi katika Kaunti ya Kisii Evans Gesanda, amewashauri wazazi kusaidia watoto wao katika ukuzaji wa vipawa na talanta.
Wito huo umetolewa baada ya kugunduliwa kuwa vipaji vimefanya wengi kujinufaisha kimaisha na kujiendeleza.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumapili mjini Kisii, Gesanda aliwaomba wazazi kutopuuza vipawa vya wanao vinavyochipuka wakiwa bado wachanga.
“Sisi sote kama wazazi tukikuza vipawa na talanta za watoto wetu nawahakikishia kuwa tutawawezesha watoto wetu kufika mbali maishani,” alisema Gesanda.
Aliongezea: “Idadi kubwa ya watu nchini wanatumia vipawa kama vitega uchumi maishani mwao na wengi wao wameweza kuwapeleka wanao na jamaa zao hadi vyuo vikuu. Talanta hulipa vizuri ndio maana naomba wazazi kuunga mkono ukuzaji wa vipawa katika Kaunti yetu ya Kisii.”
Gesanda alisema kuna wazazi ambao huzima talanta za wanao punde tu zinapochipuka huku wakikosa kujua kuwa talanta hizo ndizo zitawasaidia nyakati zijazo.
“Naomba tuache watoto wacheze mpira, wakimbie na wajihusishe na michezo mbalimbali. Tusiwe wepesi wa kuwakanya watoto wetu kucheza mchezo fulani. Huenda hicho ndicho kipawa chake maishani,” alisema Gesanda.