Share news tips with us here at Hivisasa

Mwenyekiti wa chama cha wazazi katika kaunti ya Nyamira Vincent Mbura na wazazi wengine wametishia kuelekea mahakamani kushtaki serikali kwa kuwasababishia hasara.

Wazazi hao wamedai serikali inasababisha hasara kwani wamewalipia wanao karo za shule ilhali walimu hawaendi shuleni kufuatia  mgomo unaoendelea nchini kulalamikia kutolipwa nyongeza ya mshahara wao.

Akizungumza na waandishi wa habari mnamo siku ya Jumatatu katika mji wa Nyamira, mwenyekiti huyo wa wazazi alisema tayari wamelipa karo ambayo hawaterejeshewa baada ya mgomo kufikia kikomo.

Mbura amesema wataenda mahakamani kutafuta haki ya kurudishiwa pesa zao, kwani serikali ina makosa kwa kutowalipa walimu ili warudi shuleni  na kuwafunza wanao.

Kulingana naye, serikali imekiuka uamuzi wa mahakama kuu ambayo iliweza kuagiza walimu kulipwa nyongeza yao ya mshahara kwa asilimia 50 hadi 60.

“Tutashtaki serikali ili itulipe karo yetu maana imetusababishia hasara kwetu. Wengine tulilipa pesa kupitia benki, wanafunzi wakaenda shule na wakarudi nyumbani kwa ukosefu wa walimu, na hiyo ni gharama nyingine ya nauli serikali lazima wakati huu itulipe sisi wazazi,” alihoji Mbura.

"Muhula wa kwanza wanafunzi walikosa kufunzwa wiki tatu mfululizo, na muhula huu wa tatu hii ni wiki ya pili, hii ni nini serikali ya Jubilee inataka kutuonyesha?”