Waziri ardhi katika kaunti ya Kisii Moses Onderi amewashauri wakazi kuhusisha wakili katika uuzaji wa mashamba.
Alisema wamiliki wa mashamba sawa na wanunuzi sharti wahusishe wakili ili kuzuia mizozo ambayo hutokana na uuzaji wa mashamba.
Onderi akiongea katika ofisi yake siku ya Ijumaa, aliwatahadharisha wakazi dhidi ya kuuza ardhi kiholela bila ya makubaliano rasmi. Hali hii alisema imekuwa ikileta ugomvi baina ya watu.
Waziri huyo aliwaomba wahusika kuwa makini wanapohusika na biashara kama hiyo.
"Ni muhimu wakili kuidhinisha makubaliano ya pande zote mbili ili kunapotokea ugomvi baadaye kuwe na thibitisho kortini iwapo itabidi suala kama hilo kutaka utatuzi wa mahakama," waziri Onderi alishauri.
Aidha, aliwataka wakazi wa kuwa huru kuitembelea afisi yake au idara ya usajili wa ardhi ili kupata ushauri jinsi ya kushughulikia masuala ya ardhi.
Waziri amesema haya siku chache baada shule moja ya binafsi kuchomwa na watu wasiojulikana kwa kile kinachodaiwa kuwa mzozo wa shamba.