Zaidi ya vijana 95 katika eneo la pwani waliyoathirika na utumizi wa dawa za kulevya wamejiwasilisha kwa mashirika ya kijamii na viongozi wa kaunti za pwani kupata usaidizi na kujinasua katika janga hilo.
Vijana hao waliyopokelekwa na Gavana wa kaunti ya Mombasa Hassan Ali Joho, na Mwenyekiti wa Shirika la kijamii la ‘Lamu Youth Alliance’ Wallid Ahmed siku ya Jumatano mjini Mombasa, wamesema kuwa wamekubali kujiwasilisha kwa mashirika na viongozi wa kaunti ili wasaidiwe kujinasua kutoka kwa janga hilo.
Baadhi ya vijana hao walisema kuwa wamekuwa wakitumia mihadarati aina tofauti kwa muda wa miaka zaidi ya 15 licha ya kupitia changamoto nyingi za kukabiliana na maafisa wa polisi na raia.
“Tumetumia dawa za kulevya ambazo hata zingine hatuzijui majina kwa zaidi ya miaka 15, lakini sasa tumeamua sisi wenyewe tujilete hapa kwa viongozi na mashirika haya ya kijamii yatusaidie. Tunapitia mateso mengi wala sio kupenda kwetu. Maisha ndio yametupeleka hivi,” alisema mmoja wa waathiriwa hao.
Waathiriwa hao wamewataka viongozi wa kaunti na wale wa mashirika ya kijamii kujitokeza na kuwasaidia katika kuwapa matibabu pamoja na kuwapeleka katika vituo vya kuwarekebisha tabia waraibu wa mihadrati.
Aidha, wameahidi kutorejelea uraibu huo endapo viongozi hao na wahisani watawasaidia kujinasua na kuacha kutumia dawa za kelevya.
Vijana hao wamesema kuwa watawashauri vijana wengine waliojitosa katika utumizi wa mihadarati ili kuacha na kupata matibabu maalum.
“Tunawaomba viongozi nyote milio hapa mtusaidie tutoke katika janga hili la utumizi wa mihadarati. Tumeathirika hata watuona vile tulivyo hatujui watoto wetu na wake zetu wako wapi. Tumekiri sisi wenyewe hatutatumia tena mihadarati,” alieleza mmoja wa vijana hao.
Hata hivyo gavana wa kaunti ya Mombasa Hassan Ali Joho ameahidi kushirikiana na viongozi wengine wa eneo la pwani na kuwapeleka vijana hao katika vituo vya kuwarekebisha tabia pamoja na kuwapa matibabu maalum ili kurudisha hali yao ya hapo awali.
“Wale wote watakaojitokeza ili kupata matibabu kwa kukubali kuacha kutumia dawa za kulevya basi tunawaahidi watapata matibabu kwa sababu sisi viongozi tuko tayari kuwasaidia ili mpate kupona. Serikali za kaunti ziko na nafasi nyingi za kazi. Wakati wataalam watakaposema mmepona basi tutawapa kazi,” alisema Gavana Joho.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirika la Kijamii la 'Lamu Youth Alliance', Wallid Ahmed, aliahidi kushirikiana na viongozi wa kaunti pamoja na mashirika mengine ya kijamii yatakayojitokeza katika kuwasaidia vijana waliyoathirika kujinasua.
Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa kujizatiti katika kujenga vituo vya kurekebisha tabia ya wathiriwa wa utumizi wa dawa za kulevya eneo la pwani, ili kuona kwamba idadi ya vijana waliyojitosa katika janga hilo inapungua kwa asilimia kubwa.
Kwa sasa vijana hao wanaendelea kupata ushauri pamoja na matibabu katika kituo cha kurekebisha tabia cha shirika la kupambana na utumizi wa dawa za kulevya pwani la Reachout Centre Trust eneo la Mtongwe na wengine wakipelekwa katika kituo cha eneo la Miritini.