Askofu wa dayosisi ya Kisii Joseph Mairura amesema kuwa ziara ya Papa Francis nchini Kenya italeta umoja na amani.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne mjini Kisii, Askofu Mairura alisema kuwa Papa Francis na matumaini ya kuwaunganisha Wakenya kwa amani.
Mairura aliomba Wakenya kuendelea kuombea safari ya papa mtakatifu ili afike vizuri humu nchini na kuleta amani.
Askofu Mairura alisema Papa Francis anapozuru nchi fulani, yeye huwahimiza wananchi kuwa na moyo wa kusameheana.
“Ziara ya papa mtakatifu nchini italeta amani na upendo, na wale wanaofikiria kuwa atakuja kutenganisha na kugawanya wananchi wanakosea. Nia ya ziara ya papa mtakatifu ni kuleta amani miongoni mwa Wakenya,” alisema Mairura.
Askofu huyo alisema wamejitayarisha vilivyo kumlaki Papa Francis kwa njia ya heshima na upendo.
Aidha, Mairura aliwaomba wakazi kuwa na moyo wa kusaidia wenzao kama njia moja ya kuleta upendo na amani.