Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Huku zoezi la kuwapa chanjo watoto walio na umri wa mwaka mmoja hadi tano ukianza siku ya Ijumaa, baadhi ya wakazi kutoka eneo la Jogoo mjini Kisii wameonekana wakishirikiana na wahudumu wa afya ambao wanaendelea kutekeleza zoezi hilo.

Mmoja wa wahudumu wa afya ambaye alihakikisha shughuli hiyo inaendelea katika eneo zima la Coke na Kari, viungani mwa mji wa Kisii Bi Nancy Adhiambo, alisema kuwa zoezi limeendelea salama, huku akisema wengi wa wazazi wameitikia wito na walikuwa tayari kuwasilisha watoto wao ili kupata chanjo hiyo.

Hata hivyo, alisema bado waumini na washirika wa jumuia ya wakatholiki wamepinga na baadhi yao kususia kuleta watoto wao katika zoezi hilo, huku wakidai kuwa sharti wapewe ufahamu wa kutosha na viongozi wao wa kanisa au wapewe ufahamu wa kutosha na wizara ya afya.

“Wengi ambao wanaonekana kuleta pingamizi na wa kanisa la kikatholiki, lakini baadhi yao wameshawishika na kuleta watoto wao kupewa chanjo hiyo, tunawasihi wakazi wa eneo hili wasidanganywe na yeyote kuhusiana na zoezi hili kwa vile linalenga kuwafaidi watoto dhidi ya kupooza,” alisihi mhudumu huyo.

Bi Adhiambo alitoa matumaini kuwa zoezi hilo litafaulu kwa ushirikiano baina ya wazazi na walezi wa watoto husika na kuwataka wote waunge mkono zoezi hilo la chanjo ya polio ambalo litaendelea kwa siku tano zijazo.