Huku zikisalia siku chache kwa uchaguzi mdogo wa Malindi kufanyika, imebainikia kuwa asilimia 40 ya vijana mjini Malindi wameathirika na utumizi wa dawa za kulevya, hali ambayo imetajwa kuchangia kuwepo na idadi ndogo ya vijana waliojisajili kama wapiga kura.
Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne katika mkutano wa hamasa kuhusu kujitenga na mihadarati, aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Abubakar Badawy alisema kuwa hatua hiyo imezorotesha utekeleza wa miradi mabalimbali ya kiamendeleo.
Badawy alisema kuwa wagombea wa kiti cha eneo bunge hilo wanafaa kuangazia swala hilo kwani vijana wengi wanaelekea kuangamia na huenda eneo bunge hilo likakosa vijana katika siku za usoni, iwapo swala hilo litakosa kuangaziwa.
Aidha, alisema kuwa ukosefu wa ajira, kushuka kwa sekta ya utalii na uvuvi katika eneo hilo ndio chanzo kikubwa cha vijana kujiunga na maswala ya mihadarati katika maeneo ya Maweni, Shella na Mbuyu.
"Tunasema kuwa hali hii ya vijana kushiriki katika utumizi wa mihadarati inaathiri pakubwa maendeleo ya eneo bunge la Malindi na imechangia pakubwa kuorodhesha idadi ndogo ya vijana wanaojisajili kama wapiga kura. Tunawataka viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi huu mdogo ujao kuhakikisha kuwa wanawasaidia vijana hawa kujitoa katika jinamizi hilo,” alisema Badawy.
Eneo bunge la Malindi linawapiga kura 53, 853 wanaotarajiwa kushiriki katika uchaguzi huo mdogo wa tarehe 7 mwezi Machi, idadi ambayo imetajwa kuwa ndogo mno ikilinganisha na idadi ya wakaazi wanaoishi katika eneo bunge hilo.