Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakaazi wa eneo bunge la Mvita wametakiwa kutumia siku chache zilizosalia kujisajili kuwa wapiga kura kwa lengo la kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao.

Kulingana na mbunge wa eneo hilo Abdulswamad Shariff Nassir, hali ya wakaazi kusubiri hadi nyakati za mwisho wa zoezi hilo imekuwa desturi na kuchangia wengi kufungia nje na kushindwa kusajiliwa na akadokeza kwamba ni lazima wakaazi wajitokeze mapema ili washiriki kikamilifu zoezi hilo.

Akizungumza katika eneo bunge lake la Mvita mjini Mombasa siku ya Jumatano, Abdulswamad alisema kwamba japo zoezi hilo limekumbwa na changamoto ya uhaba wa vifaa vya kuwasajili wapiga kura kwa njia ya kieletroniki, wakaazi hao wana uwezo wa kufuatilia jinsi zoezi hilo linavyotekelezwa ili wasiwachwe nje bali wasajiliwe mapema.

Mbunge huyo amehoji kwamba alikuwa akiendeleza kampeni za kuwarai wakaazi kujitokeza ili wasajiliwe kama wapiga kura na juhudi hizo zitaendelezwa katika kila pembe ya eneo bunge hilo la Mvita hadi pale zoezi hilo litakapokamilika.

"Ninawaomba tafadhali wakaazi wa Mvita jitokezeni kwa wingi mjisajili kuwa wapiga kura ili mshiriki kikamilifu katika shughuli ya uchaguzi mkuu ujao badala ya kusali kimya hadi siku za mwisho za zoezi hilo ndio mjisajili hiyo itakuwa mumechelewa na huenda mkakosa kusajili na kuwa vigumu kubadili uongozi duni," alisema Abdulswamad.

Zoezi hilo la usajili wa wapiga kura ambalo limetengewa muda wa siku 30 na tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka nchini IEBC litakamilika Jumanne ijayo, huku wakaazi wa Pwani wakihimizwa kutumia muda uliyosalia ili kusajiliwa kama wapiga kura.