Wahudumu wa magari mjini Kisii wamelaumiwa vikali na wakaazi kwa madai ya kubeba mizigo kupita kiasi na hivyo kuhatarisha maisha ya abiria.
Wakaazi hao wanasema wahudumu hao wamekosa kutii sheria za trafiki huku wasafiri wakizidi kuumia kutokana na huduma mbaya.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Ijumaa mjini Kisii, abiria waliwakosoa wakisema kuwa hawajali maisha ya binadamu na kuwataka maafisa wa polisi kuhakikisha sheria za usafiri zinazingatiwa.
“Jinsi wahudumu wa matatu hubeba mizigo mingi huenda tukasababishiwa madhara makubwa iwapo maafisa wa polisi hawatakuwa makini,” Divinah Moseti alisema.
“Baada ya kupanda gari wengine hufunga mlango wa gari na kuanza kuweka mizigo mingi kwa bodi na kuifunga kwa kamba mpaka tunaogopa , tunapowakanya wanasema gari ni ya umma tununue zetu za kibinafsi,” Joseck Morara alisema.
Sasa abiria hao wanaitaka idara ya trafiki mjini Kisii ihakikishe kuwa magari yote ya umma yanazuiwa kubeba mizigo hiyo.