Kulishuhudiwa mlolongo mkubwa siku ya jumanne vituo vya kuabiri mabasi mjini Mombasa huku baadhi ya abiria wakilazimika kurejea nyumbani kutokana na ughali wa nauli.
Pia kulikosekana tiketi za kusafiria kufuatia idadi kubwa ya wasafiri.
Wengi wa abiria waliokosa kusafiri wamelalamikia hatua ya wenye magari kupandisha nauli maradufu huku wakitaja hatua hiyo kama unyanyasaji kwa wasiojiweza katika jamii.
''Kwa kawaida kutoka Mombasa hadi Nairobi hua tunalipishwa kati ya shilingi elfu 1000 - 800, leo hii wanakata tiketi kati ya Sh1,500-Sh2,000. Jameni hii si ni hujuma!'' alisema mmoja wao aliyejawa na ghadhabu.
Abiria hao sasa wanataka serikali kutathmini umbali wa safari na kisha kuweka kiwango maalum ambacho kila mtu atalipishwa bila kujali msimu au wakati.
Inadaiwa wenye magari wanalenga kuvuna msimu huu wa Krismasi kwa kupandisha nauli kutokana na idadi kubwa ya abiria wanaosafiri sehemu mbalimbali nchini kujiunga na familia zao wakati huu wa siku kuu.
Haya yanajiri siku moja tu baada ya idara ya trafiki Pwani kuwahimiza abiria kuwa makini na uhalali wa magari wanayoabiri ili kuepuka kulaghaiwa.