Share news tips with us here at Hivisasa

Huku halmashauri ya uchukuzi na usalama barabarani ikiendelea kukaza kamba dhidi ya wahudumu wa matatu kote nchini, abiria kutoka Kaunti ya Mombasa wamelalamikia kuwepo michoro mibaya na kuonyeshwa video zilizokosa maadili kwenye magari mengi ya abiria.

Abiria hao ambao waliongea na mwandishi huyu wa habari siku ya Jumatano kwenye baadhi ya steji za magari jijini humo waliwalaumu madereva wa magari ya abiria kwa kucheza miziki yenye sauti na kuonyesha video zenye maungo wazi ya wasanii na wacheza densi.

Leila Mwakio, ambaye ni mfanyakazi katika duka moja la kuuza nguo jijini Mombasa alisema kuwa imekuwa vigumu kwake kupanda magari kama hayo, akisema kuwa inambidi kuhiari kutumia magari madogo maarufu kama Tuk Tuk ambazo alisema kuwa angalau hazina kelele na picha mbaya.

“Mimi nina watoto wadogo ambao ninawapeleka shuleni, na filamu pamoja na miziki inayochezwa kwenye matatu zetu ni za kusononesha na hazina maadili, sharti idara ya trafiki ichukue nafasi hiyo kuawadhibu wote wanaovunja sheria,” alisema mama huyo.

Salim Karim, mhudumu wa klabu kimoja mjini Mombasa aliunga mkono msako huo wa halmashauri ya uchukuzi na usalama wa barabara nchini huku akisema kuwa hatua hiyo ingechukuliwa kitambo.

Hata hivyo, baadhi ya wahudumu hao walipinga madai hayo wakisema wao hufanya hivyo kuwaburudisha abiria wao wanaposafiri.