Wasafiri wanaopania kusafiri kuelekea mji mkuu wa Nairobi watalazimika kugharamikia nauli zaidi baada ya nauli kupanda katika mashirika tofauti yanayotoa huduma za usafiri.
Wakizungumza kwenye maeneo ya magari ya usafiri wa umma mjini Nakuru, wamesema nauli imepanda maradufu na huenda wengi wakashindwa kusafiri.
Joyce Adeko, ambaye alitarajia kusafiri kutoka Kitale hadi Nairobi amesema amejuta kupanga safari yake msimu huu akisema ameisitisha kwa ghafla na atalazimika kusherehekea krismasi yake mjini Nakuru.
“Siwezi nikasafiri kwa bei hiyo kwani ni hujuma, nina watoto wanne, toka kitale nimetumia 4,500 na siwezi ongeza 4,700 zaidi kwani hata sina hela hizo, ” Adeko alisema.
Hatua za kuwasiliana na msemaji wa Mololine tawi la Nakuru hazikufua dafu kwani hakua ofisini wala kuchukua simu.
Hata hivyo madereva wanaohudumu katika vituo hivyo vya magari ambao hawakutaka kutajwa majina yao kwa minajili ya usalama wa kazi yao, wamesema bei ya petroli ni ghali mno na sheria mpya za usafiri zinawafanya kuongeza nauli.