Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kulizuka kioja katika kituo cha kibiashara cha Maseno mjini Subukia siku ya Jumatatu, baada ya afisa wa kitengo cha AP aliyekuwa mlevi kuvuruga mkutano wa nyumba kumi huku akitishia kupiga risasi waliokuwemo miogoni mwao akiwa naibu kamishna wa kaunti.

Afisa huyo wa ngazi ya sajini (sergeant) alifika kwenye eneo la mkutano huo katika kambi ya chifu iliyo kwenye eneo la Wei akiwa mlevi, kabla ya kuelekea moja kwa moja hadi kwa nyumba yake ambapo alitoka huku akiwa ameshika bunduki yake, hatua iliyopelekea waliokuwemo kwenye mkutano huo kukimbilia usalama wao.

Baadhi ya watu walijeruhiwa kwenye kioja hicho wakijaribu kuruka ua lililokuwa limezingirwa kwa seng’enge karibu na kambi hiyo ya chifu.

Waliohojiwa na wanahabari walikariri kuwa afisa huyo alikuwa mlevi siku yote Jumapili, na kufikia Jumatatu asubuhi, bado alikuwa akibugia vileo.

Kioja hicho kilipelekea biashara kusitishwa kwa muda huku baadhi ya watu wakiangalia kilichokuwa kikijiri kutoka mbali huku polisi wakimwomba mwenzao aliyekuwa mlevi kuwapa bunduki yake.

Punde tu aliposalimu mwito huo na kusalimisha bunduki yake, afisa huyo alipelekwa hadi katika makao madogo makuu ya kitengo cha AP yaliyo Subukia (Subukia Sub county AP headquarters) ambapo alihojiwa.

Tukio hilo sasa limepelekea wakazi wa eneo hilo kulaumu unywaji wa pombe haramu kwa tukio hilo, wakisema afisa huyo ambaye hajakaa kwa kambi hiyo kwa mwezi mmoja ana mazoeaa ya kubugia pombe hiyo.

Huku akitaka hatua kali ichukuliwe dhidi ya afisa huyo, mwakilishi wa wadi ya Weseges Njeng’a Kang’ethe alisema kwamba afisa huyo alipewa uhamisho kutoka kwa kituo kidogo cha polisi cha Mbogo-Ini kutokana na mazoeaa ya unywaji pombe na madai ya kuitisha hongo.

Amesema kuwa ni aibu kwa mtu yeyote ambaye ametwikwa wajibu wa kukabiliana na pombe haramu na lile la kuhakikisha watu wanasalia salama kujiendesha kwa njia hiyo hadharani.