Share news tips with us here at Hivisasa

Huku ikisalia wiki moja kabla ya kufunguliwa kwa shule kote nchini, afisa wa elimu kutoka jimbo la Nakuru Joseph Tonui amesema idadi ya watoto wengi wanaweza kukosa kurejea shuleni baada ya kuathirika na mzozo unaozidi kushuhudiwa kati ya jamii mbili katika eneo la Olposimoru, kwenye mpaka wa jimbo la Nakuru na lile la Narok.

Aidha, imebainika kuwa mzozo huo umepelekea zaidi ya familia 500 kutoroka katika eneo hilo, huku ikiwabidi kupiga kambi katika shule ya upili ya Olenguruone DEB.

“Ipo haja kwa serikali kuu na za kaunti kufuatilia na kuhakikisha kuwa suluhu la kudumu limepatikana kwa mzozo huu ili kuwezesha watoto wa shule kurejea shuleni kwa wakati unaofaa,” alisema Tonui baada ya kuwatembelea na kuwapa msaada waathirwa hao siku ya Jumapili.

Tonui ameyasema haya huku mali ya waathiriwa hao zikiwemo sare za shule na hata vitabu vilitekeketea wakati wa vuta nikuvute iliyoshuhudiwa wakati wa mzozo huo.