Kufuatia idadi ndogo ya wakazi wanaojitokeza kwenye vituo vya kusajili wapiga kura kote nchini, naibu mshirikishi wa Tume ya IEBC katika Kaunti ya Nyamira Rosemary Obara amebuni mbinu itakayo hakikisha kuwa idadi kubwa ya wapiga kura wanasajiliwa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye mahojiano na wanahabari siku ya Jumatano, Bi Obara alisema kuwa maafisa wa usajili wa tume hiyo wataanzisha mikakati ya kutembelea soko, maeneo ya hafla za mazishi na hata pia hafla za kuchangisha pesa, ili kufikia idadi kubwa ya wapiga kura.

"Kwa kweli tumekuwa tukishuhudia idadi ndogo ya wananchi wanaojitokeza kwenye vituo vya kusajili wapiga kura na ndio maana tumebuni mikakati ya kuanza kutembelea maeneo ya harambee, hafla za mazishi na hata pia soko mbalimbali, ili kuwafikia watu wengi. Kufikia sasa naona kama mbinu hii imetusaidia pakubwa," alisema Bi Obara.

Obara aidha alisema kuwa mbinu hiyo itawasaidia kuafikia idadi ya watu wapatao elfu 300,000, idadi ambayo tume ya IEBC inatarajia kusajili katika kaunti hiyo.

"Naona kwamba mbinu hii mpya huenda ikafanikiwa na ni ombi langu kwa kwa maafisa wetu wa usajili kuhakikisha kwamba wanazingatia hili kwa maana tunataka kuafikia idadi kubwa ya watu tunaonuia kuwasajili. Hili suala la kusajili watu elfu 300,000 halitakuwa changamoto kwetu," alisema Obara.

Bi Obara aidha aliwahimiza maafisa wa utawala hasa machifu na manaibu wao kushirikiana kikamilifu na tume ya IEBC ili kuhakikisha kuwa mpango wa kusajili Wakenya kama wapiga kura unafanikiwa.

"Sisi kama tume ya IEBC hatuwezi fanikiwa pekee yetu kwenye shughuli hii ya usajili wa wapiga kura na ndio maana nawaomba maafisa wa utawala kushirikiana na maafisa wetu wa usajili ili kufanikisha shughuli hii," alisema Obara.