Aliyekuwa afisa wa wanyama pori na wenzake wawili wamefunguliwa mashtaka kwa kupatikana na risasi 54 kinyume cha sheria.
Upande wa mashtaka uliambia mahakama siku ya Juamatatu, kuwa mnamo Disemba 30, 2015, mshtakiwa, Mohamed Hussein Warsame, ambaye alihudumu kama afisa wa KWS, Aden Abdalla Abdi na Roble Kassim Abdi walikamatwa katika eneo la Bondeni wakiwa na risasi 54 zinazoaminika kutumika kutekeleza uhalifu.
Washukiwa hao watatu wa uhalifu waliokamatwa na risasi 54 katika hoteli moja ya kukodi katika eneo la Bondeni, walisomewa mashtaka baada ya uchunguzi wa siku 30 kukamilika.
Watatu hao walikanusha mashtaka hayo mbele ya Hakimu Richard Odenyo.
Mahakama iliwanyima dhamana baada ya idara ya KWS kuwasilisha ombi la kuzuiliwa kwa watatu hao, kwa kusema kuwa Mohamed Warsame anakabiliwa na mashtaka sawia na hayo katika mahakama ya Nyanyuki.
Kesi hiyo itasikizwa Machi 4, 2016.