Share news tips with us here at Hivisasa

Chuma cha afisa wa polisi ambaye alikodisha gari lake kwa wavulana watano waliofariki katika ajali eneo la Salgaa barabara ya Eldoret-Nakuru ki motoni, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Keriako Tobiko kuamuru uchunguzi ufanywe na kukamilishwa haraka.

Siku hiyo jumla ya wavulana wanane walipoteza maisha yao katika eneo hilo hatari na maarufu kwa ajali za barabara.

Tobiko alisema ataamua iwapo atamfungulia mashtaka afisa wa polisi wa utawala ambaye gari lake lilitumiwa na wavulana hao ambao waliaga dunia mkesha wa mwaka mpya.

Mbali na afisa huyo wa usalama, vilevile Tobiko atatoa mwelekeo iwapo wenye vilabu vya kuuza pombe ambapo vijana hao walijivinjari wakibugia tembo kabla ya kuangamia katika ajali watachukuliwa hatua kwa kuwauzia watoto pombe.

Tobiko aidha alisema polisi wanajua kwamba wanatakiwa kukamilisha zoezi la upelelezi na mahojiano kwa haraka.

Agizo hilo la DPP lafuatia amri ya mamlaka ya kitaifa kupambana na unywaji wa vileo (Nacada) kuamuru vilabu vitatu ambako wavulana hao waliuziwa pombe kabla ya kufariki kwenye ajali vifungwe kabisa.

Tobiko alithibitisha kwamba aliamuru wiki hii uchunguzi ufanywe kwa haraka na kukamilishwa kisha ripoti ipelekwe ofisini mwake.

Kitakachoangaziwa katika uchunguzi huo ni jinsi gari hilo lenye nambari za usajili za kigeni lilikodishiwa wavulana hao ilhali halikuwa taksi.

Wapelelezi pia watawahoji wamiliki wa baa tatu mjini Nakuru ambapo wavulana hao walilewa chakari kabla ya kuanza safari iliyoishia mauti eneo hatari la Salgaa ambapo maelfu ya watu wameangamia.

“Uchunguzi wa kina utafanywa kutambua kutambua sababu gari hilo la afisa wa polisi lilikuwa na nambari za usajili za kigeni. Aliyekodisha gari hilo atatambuliwa sawia na wenye vilabu ambapo watoto hao waliuziwa pombe,” alisema Tobiko.