Maafisa wa tume ya kukabiliana na ufisadi eneo la kusini mwa Bonde la Ufa siku ya Alhamisi waliwatia mbaroni afisa mmoja wa polisi pamoja na dereva wa teksi waliokuwa wakiitisha hongo kwa wafanyibiashara wawili wa dhahabu yenye thamana ya shilingi milioni 1.9 katika eneo la Busia.
Afisa huyo mwenye cheo cha Koplo Fredrick Sherlif na mwenzake walitiwa mbaroni wakiwa kwenye hoteli moja mjini Nakuru ambapo walikuwa wakistarehe baada ya mtego wa maafisa hao kufaulu.
Gilbert Lukhonga, ambaye ni naibu mkurugenzi wa shirika hilo la EACC katika eneo hilo alisema walalamishi walipiga ripoti kuhusu wawili hao walipowashuku baada ya kuitishwa hongo ya shilingi elfu mia tatu.
“Tutafanya upelelezi wetu kwa kina, na kuwafikisha mahakamani,” alisema Luhkonga
Hata hivyo, Lukhonga amewahimiza wananchi kuripoti visa vyovyote vya hongo kwa maafisa wake, akitaja ufisadi kuwa kero kubwa nchini na amblo limekwamisha maendeleo ya taifa la Kenya.