Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma ameagiza kuondolewa mashtaka na kuachiliwa huru kwa mwanabloga Antony Waime Mburu anayekabiliwa na madai ya kumuharibia jina Gavana wa Kiambu William Kabogo.

Kupitia kwa naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa Alexendra Muteti ameitaka mahakama kumwachilia huru mshukiwa baada ya polisi kukosa kuwasilisha ushahidi wa kutosha ili kumfungulia mashtaka hayo.

Muteti aliambia mahakama kuwa aliagizwa na mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma nchini Keriako Tobiko kumuondolea mashtaka na kumuachilia huru mwanabloga huyo.

Hatua hii inajiri baada ya wakili wa mwanabloga huyo, Adalla Boaz kuomba mahakama siku ya Ijumaa kutaka mteja wake kuondolewa mashtaka hayo kwa kile alichokitaja kuwa ukandamizaji wa uhuru wa wanahabari.

Mwanabloga huyo anadaiwa Januari 8, 2016 aliandika taarifa inayomuhusisha Kabogo kuwa anafanya biashara ya mayai yenye bei ya chini, hali aliyoitaja kukandamiza na kuharibu biashara ya uuzaji mayai nchini.

Aidha, anakabiliwa na mashtaka matatu huku jengine likiwa ni la kutumia vyombo vya mawasiliano vibaya.

Mwanabloga Mburu atasalia korokoroni hadi Jumanne wiki ijayo kusubiri uamuzi wa kuachiliwa kwake huru.