Wajumbe wa vuguvugu la Maendeleo Chap Chap lililo zinduliwa na Gavana wa Kaunti ya Machakos Alfred Mutua katika Kaunti ya Mombasa, wamebaki na mshangao baada ya watu wasiojuliukana kufuta jina la ofisi hiyo ilioko eneo la Changamwe usiku wa kuamkia siku ya Jumanne.
Faustine Makenga, mmoja wa maafisa wakuu wa vuguvugu hilo alikemea vikali kitendo hicho, na kuwaonya watu wasiopenda maendeleo na walio na tabia ya kuwatumia vijana kutekeleza uhalifu kwa misingi ya kisiasa, akisema tabia hizo zimepitwa na wakati.
Kwa upande wake, Patricia Mutheu, ambaye ni mjumbe katika chama cha TNA eneo la Changamwe, aliwataka wananchi kutokubali kutumiwa vibaya na viongozi.
Mutheu aliwataka wakaazi kuheshimu maamuzi ya kila Mkenya, kwa kuzingatia uhuru wa demokrasia, kwa ajili ya kufanikisha maendeleo katika maeneo yote ya taifa.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya Gavana wa Machakos Alfred Mutua kuzindua rasmi afisi ya vuguvugu hilo huko changamwe, lengo kuu likiwa ni kuleta maendeleo karibu na mwananchi mashinani.