Huzuni ilitanda mapema Ijumaa katika eneo la Omogonchoro kwenye barabara kuu ya Nyamira-Kisii baada ya gari dogo la wazima moto kutoka kaunti ya Kisii kuhusika kwenye ajali ya barabarani iliyosababisha maafa ya dereva wa gari hilo papo hapo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akithibitisha kisa hicho, afisa mkuu wa polisi wa Nyamira Ricoh Ngare alisema gari hilo lililokuwa likitoka mjini Kisii kuelekea upande wa Nyamira lilipoteza mwelekeo na kubingiria mara kadhaa kabla ya kusababisha ajali hiyo iliyomtoa uhai dereva. 

"Ajali hiyo ilitokea pale ambapo gari hilo lililokuwa likitoka Kisii kuelekea Nyamira lilipobingiria mara kadhaa na kusababisha kifo cha dereva wake papo hapo," alisema Ngare. 

Ngare aidha alisema manusura wawili waliokuwa kwenye gari hilo pamoja na mwenda zake wamekimbishwa kwenye hospitali kuu ya Level six kule Kisii kwa matibabu, huku mwili wa dereva ukipelekwa kuhifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Kisii. 

"Tayari manusura wawili waliokuwa kwenye gari hilo wamekimbishwa kwenye hospitali kuu ya Kisii kwa matibabu huku mwili wa mwendazake ukihifadhibiwa kwenye chumba chakuhifadhi maiti cha hospitali kuu ya Kisii," aliongezea Ngare.