Francis Ngige Ng’ang’a, aliyekuwa kijana wa kurandaranda mitaani mjini Nakuru, ameibuka kwa ushindi na kupata alama 423 katika matokeo ya mtihani wa darasa la nane KCPE ya mwaka jana.
Akizungumza na wanahabari katika shule hiyo, Ng’ang’a ambaye alisomea katika shule ya msingi ya Pema Victorius Academy na kufadhiliwa na huduma ya dhehebu la Victorius Community Church iliyo katika eneo la Mbaruku viungani mwa mji wa Nakuru, alielekeza ushindi wake kwa mungu kwa kumtoa katika mavumbi.
Aidha, alisema kuwa ushindi huo unatokana na maombi, bidii na nidhamu, huku akitazamia kuwa wakili katika siku za usoni.
Hata hivyo, msimamizi wa shule hiyo na ambaye pia ni askofu wa dhahebu la Victorius Community Church, Jackson Maina Mwangi alisema kuwa ni wito ambao amekuwa nao tangu miaka ya sabini hadi wa leo ya kuwasaidia wale ambao hawajiwezi katika jamii.
Kutokana na matokeo hayo, askofu Mwangi alipongeza jitihada za waalimu miongoni mwa wengine ilikuona alama za shule hiyo zimeimarikia kutoka 320 mwaka wa 2014 hadi 337 mwaka wa 2105.
Aliahidi kuendelea kuwasaidia watoto hao hadi pale watakapoweza kujitegemea wenyewe.
Vile vile aliahidi kujenga vituo vya kiufundi anuai ili kuwasaidia wale ambao kimasomo hawakufauli, kama njia moja ya kuisaidia serikali kuwapa taaluma vijana.
Haya yanajiri baada ya waziri wa elimu Fred Matiang’i kutangaza matokeo ya mtihani ya darasa la nane KCPE jumatano wiki hii, huku akisema kuwa shule za msingi za umma zilifanya vibaya ikilinganishwa na zile za kibinafsi.