Iwapo itabainika kuwa jaji Phillip Tunoi alipokea hongo ya shilingi milioni 200 kutoka kwa gavana wa kaunti ya Nairobi Dakta Evans Kidero ili aweze kuwashawishi wenzake kutoa uamuzi utakaoegemea upande wa gavana huyo katika kesi ya kupinga uchaguzi wake, ni vyema kwa majaji wa mahakama ya upeo waliohusika katika kesi hiyo kupigwa kalamu.
Huo ni usemi wake mbunge wa Nakuru Magharibi Samwel Arama aliyesema hatua hiyo inafaa kuchukuliwa iwapo itabainika hongo hiyo ilitolewa kwani majaji wote waliohusika katika kesi hiyo waliegemea upande wa Kidero.
Ni matamshi ambayo alitoa siku chache baada ya kamati maalum iliyobuniwa na tume ya Huduma za mahakama JSC chini ya uenyekiti wake Margaret Kobia kupendekeza kwa Rais Uhuru Kenyatta kuchunguzwa kwa jaji Tunoi baada ya ripoti kuhusiana na uchunguzi wao kubaini kwamba kulikuwa na mawasiliano baina ya upande wa Kidero na jaji Tunoi.
Aidha, mbunge huyo alimsuta jaji mkuu Willy Mutunga kwa kusubiri kwa muda mrefu bila kuweka bayana kwamba alipokea malalamishi dhidi ya jaji Tunoi.