Mbunge wa Nakuru magharibi Samuel Arama amewaonya vikali maafisa wa umma wanaotumia pesa zilizotengwa kufadhili miradi ya umma kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubia na wanahabari kwenye hafla ya kuchangisha pesa za kujenga hospitali ndogo ya Borabu siku ya Ijumaa kule Nyansiongo, Arama alisema kuwa afisa yeyote wa umma atakaye patikana na hatia ya kuvuja pesa za miradi ya umma atachukuliwa hatua kali za kisheria. 

"Kuna maafisa wenye mazoea yakuvuja pesa za umma zilizotengwa kufadhili miradi muhimu, na kwa ukweli iwapo kutakuwa na ushahidi wa kuwatuhumu maafisa husika pasina shaka watafunguliwa mashtaka na kufungwa gerezani," alionya Arama. 

Arama aliongeza kwa kusema kuwa anatumai kuwa bodi ya hospitali ndogo ya Borabu itatumia shillingi millioni kumi zitakazotolewa na serikali ya kaunti ya Nyamira kwa njia inayostahili ili kustawisha hospitali hiyo hata zaidi. 

"Natumai kuwa bodi ya usimamizi ya hospitali hii itawajibikia shillingi millioni kumi zitakazotolewa na serikali ya kaunti ya Nyamira ili kufadhili mradi huu inavyo faa ili kwamba watu wa eneo hili wafaidi kutokana na huduma zitakazo peanwa na hospitali hiyo," alisema Arama. 

Mbunge huyo aidha alisuta vikali vyombo vya habari kwa kuendelea kuchochea hisia za wananchi dhidi ya serikali ya kaunti ya Nyamira, hali aliyosema inaathiri pakubwa ukuaji wa kaunti hiyo huku akivihimiza vyombo hivyo kueneza jumbe za amani na ushirikiano ili kustawisha kaunti hiyo. "

"Haya mazoea ya baadhi ya vyombo vya habari kuendelea kusambaza jumbe za kuchochea wananchi dhidi ya serikali ya kaunti ya Nyamira ni mojawapo ya vizingiti vya maendeleo kwenye kaunti hii, na ningependa kuvisihii vyombo hivyo kueneza jumbe za ushirikiano na amani ili kusaidia kaunti hii kujistawisha," alihimiza Arama. 

Akizungumzia swala la uwajibikaji kwenye utendakazi baina ya viongozi, Arama aliwahimiza wabunge wenzake kuhakikisha kuwa wanatumia pesa za ustawishaji maeneo bunge CDF kwa miradi mhimu badala ya kuingiza siasa ya kuzikosoa serikali za kaunti. 

"Ningependa kuwasihii wabunge wenzangu kuhakikisha kuwa wanatumia vizuri pesa za maendeleo ya maeneo bunge CDF badala yakuingiza siasa ya kuzikosoa serikali za kaunti kwa kuwa majukumu ya uangalizi ni ya wawakilishi wa wadi na wala sio wabunge," alisema Arama.